Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya raia 1,500 wameuawa Iraq mwezi Juni

Familia hii ilikimbia mapigano Mosul, Iraq na wako karibu na kituo cha Khazair.Wanamatumaini ya kukakaa mji wa Erbil hadi itakapokuwa salama kurudi nyumbani(Picha@UNHCR/R.Nuri

Zaidi ya raia 1,500 wameuawa Iraq mwezi Juni

Umoja wa Mataifa umeyashutumu makundi yenye silaha nchini Iraq kwa kutekeleza vitendo vya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, mwingine ambao huenda ukawa uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Ripoti iliyoandaliwa na Ofisi ya Haki za Binadamu na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq, UNAMI, imesema kuwa raia wapatao zaidi ya 1,500 waliuawa na wengine zaidi ya 1,700 kujeruhiwa mwezi Juni pekee.

Zaidi ya raia 600,000 wa Iraq pia walilazimika kuhama makwao katika kipindi kicho hicho.

Ripoti hiyo inasema kuwa wafuasi wa kundi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iraq na Levant (ISIL) na makundi mengine chini yake, waliwalenga raia moja kwa moja, pamoja na miundo mbinu ya umma, kwa lengo la kuwaua na kuwajeruhi raia wengi iwezekanavyo.

Ofisi ya Haki za Binadamu pia imesema kuwa ina taarifa za kuaminika kuhusu usajili na utumiaji wa watoto kama wanajeshi.

Ravina Shamdasani ni msemaji wa Ofisi ya Haki za Binadamu

“Ripoti pia inabainisha uhalifu ulioetendwa na vikosi vya usalama vya Iraq (ISF) na vikosi husika. Inaeleza mahangaiko na machungu ambayo raia wanapitia, na mauaji ya halaiki, majeraha nauharibifu wa vitega riziki na mali zao”

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu, Navi Pillay, amesema kuwa ana wasiwasi hasa kuhusu ulinzi na maslahi ya makundi yaliyo hatarini, ambayo yamo katika maeneo yaliyoathiriwa na mapigano, hususan wanawake, watoto, watu wenye ulemavu, wazee na makundi ya walio wachache.