Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto 10,000 wa Syria wamezuiwa kupata matibabu: UNICEF

Watoto 10,000 wa Syria wamezuiwa kupata matibabu: UNICEF

Serikali ya Syria imezuia usambazaji wa dawa na vifaa vingine vya kujisafi kwa takriban watoto 10,000 wanaoishi katika mji uliozingirwa wa Mouadamiya al-Sham, katika eneo la Damascus, kwa mujibu wa Shirika la Kuhudumia Watoto, UNICEF.

Mji huo ulioko mwendo wa kilomita 8 kutoka Damscus, umezingirwa tangu mwezi Agosti mwaka jana, na kulingana na UNICEF, hali katika mji huo ni mbaya mno, na kumekuwa na visa vya vifo kutokana na utapiamlo miongoni mwa watu wakazi wake.

Mji wa Mouadamiya una idadi ya takriban watu 20,000. UNICEF ni miongoni mwa mashirika ya Umoja wa Mataifa ambayo yameweza kufikisha chakula na bidhaa nyingine muhimu za misaada wiki hii kwa jamii hiyo iliyozingirwa. Chris Tidey ni msemaji wa UNICEF, Geneva.

“Watoto katika eneo hilo hawajakwenda shule kwa miaka miwili iliyopita. Hofu kuu ya wazazi ni jinsi watakavywarejesha watoto wao shuleni. Kuhusu ulinzi wa watoto, tuna taarifa za watoto kusajiliwa jeshini, lakini siwezi kuthibitisha hilo kwa sasa. Kuhusu afya, kuna upungufu wa bidhaa za afya. Familia nyingi zimewajulisha wahudumu wa UNICEF kuwa hawajapata dawa wanazohitaji kwa miezi mingi. Akina mama wanaelezea hofu kuhusu watoto wao kutopata chanjo wanazohitaji.”

Ameongeza kuwa kampeni ya chanjo dhidi ya polio imepangwa kufanywa kwa ushirikiano na Shirika la Hilali Nyekundu la Syria.