UNAMA yakaribisha ukaguzi wa matokeo ya uchaguzi wa urais Afghanistan

17 Julai 2014

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan, UNAMA umekaribisha kuanza kwa ukaguzi wa matokeo ya kura ya kuwania urais wa mwaka 2014 nchini humo.

Ukaguzi huo unafuatia makubaliano yaliyokifikiwa na wagombea wawili wa urais nchini Afghanistan, Dkt. Abdullah Abdullah na Dkt. Ashraf Ghani. Makubaliano hayo yalifikiwa kwa juhudi za Waziri wa Mambo ya Nje Marekani, John Kerry.

Wagombea urais hao wawili wameelezea utashi wao wa kutoa ushirikiano na kukubaliana na matokeo ya ukaguzi huo.

Ukaguzi huo unaendeshwa na Kamisheni Huru ya Uchaguzi (IEC) chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa. Mkurugenzi wa katibu Mkuu wa kitengo cha usaidizi wa uchaguzi, Craig Jenness amewasili Kabul kusimamia maandalizi ya kuanza ukaguzi huo .

Halikadhalika, IEC inasaidiwa na wataalamu kutoka Shirika la Mpango wa Maendeleo kupitia mpango wa kukuza sheria na uwezo wa uchaguzi kwa ajili ya siku za usoni (UNDP ELECT II).

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter