Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNRWA yalaani kuwekwa kwa silaha katika shule Gaza

Watoto kutoka Yarmouk. UNRWA/Rami Al-Sayyed

UNRWA yalaani kuwekwa kwa silaha katika shule Gaza

Takriban roketi 20 zimepatikana katika shule iliyo wazi inayosimamiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwasaidia wakimbizi wa Palestina, UNRWA.

Silaha hizo zilipatikana na maafisa wa UNRWA mnamo Jumanne wakati wa shughuli za kawaida za upelelezi katika majengo yao.

Hadi sasa haijabainika ni nani alitega silaha hizo. UNRWA imelaani kitendo hicho katika shule ikiongeza kuwa ni ukiukwaji mkubwa wa haki za kimataifa kulenga majengo ya Umoja wa Mataifa

Kadhalika UNRWA imesema kwamba tukio hilo lilihatarisha maisha ya raia, wakiwemo wafanyakazi wa kibinadamu, na kuhatarisha lengo kubwa la UNRWA ambalo ni kuwalinda wakimbizi wa kipalestina walioko Gaza. Kwa sasa silaha hizo zimeondolewa na utafiti umeanzishwa.

UNRWA imeongeza kuwa imejizatiti kuhakikisha msimamo wa kutoegemea upande wowote katika majengo yake yote ikiwemo sera za kutokuwepo na silaha na upelelezi wa mara kwa mara kuhakikisha majengo yao ni kwa ajili ya mahitaji ya kibinadamu tu

Pia UNRWA imesema kwamba hadhi ya majengo ya Umoja wa Mataifa inapaswa kuheshimiwa.