Kuna matumaini ya amani CAR: Ladsous

16 Julai 2014

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Jumatano ya Julai 16 jioni limejadili kuhusu hali ya usalama nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati likiangazia maandalizi ya kuunda ujumbe wa umoja wa mataifa nchini humo, MINUSCA.

Herve Ladsous, mkuu wa idara ya operesheni za kulinda amani kwenye Umoja wa Mataifa, DPKO, amesema kwamba kuna matumaini ya kusitishwa kwa mapigano, akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuripoti mbele ya Baraza la Usalama.

Amefurahi kuona kwamba pande zote za mzozo unaoendelea  Jamhuri ya Afrika ya Kati zimekubali kuhudhuria mkutano utakaofanyika tarehe 21, Julai, mjini Brazzaville, akisema:

“ Matumaini ni kwamba wataamua kusitisha mapigano na kuweka silaha chini, ambayo itakuwa ni hatua ya kuanza kuelekea mazungumzo ya amani na maridhiano ya kitaifa ambayo yanatarijiwa kufanyika Jamhuri ya Afrika ya Kati kwenyewe. Wadau wote wa kimatifa wamejituma sana ili kufikia maamuzi hayo na wametuma ujumbe mzito wa pamoja” 

Halikdhalika amewaelezea waandishi wa habari kwamba hali ya usalama imeimarika mjini Bangui kutokana na jitahada za ujumbe wa muungano wa Afrika, MISCA na ule wa muungano wa Ulaya, lakini bado hali ni tete mikoani.

Amesema, ofisi yake inashughulikia maandalizi ya kutuma ujumbe wa Umoja wa Mataifa, MINUSCA, ambao utakuwa tayari kuanza operesheni zake katika baadhi ya sehemu za mikoani kuanzia tarehe 15, Septemba,  licha ya kwamba unakumbwa na changamoto za kufikisha vifaa kwa haraka kwenye nchi hiyo ambayo haina njia ya moja kwa moja baharini. Ameongeza kuwa anaamini MINUSCA itakuwa na nguvu za kurejesha hali ya utulivu nchini humo.