Hali ya kibinadamu dhoofu kwa maelfu Sudan na Sudan Kusini: Amos

16 Julai 2014

Mkuu wa Ofisi ya kuratibu masuala ya kibidamu na misaada ya dharura, Valerie Amos, amesema kuwa hali ya kibinadamu katika nchi za Sudan na Sudan Kusini, inaendelea kuzorota kwa mamia ya maelfu ya watu.

Bi Amos, ambaye awali amelihutubia Baraza la Usalama, amewambia waandishi wa habari mjini New York kuwa mamia ya maelfu ya watu katika majimbo ya Kordofan Kusini na Blue Nile wameendelea kuathiriwa na vita tangu azimio la Baraza la Usalama namba 2046, la Mei 2012, ambalo lilielezea masikitiko makubwa kuhusu jinsi mapigano katika majimbo hayo kati ya Sudan na SPLM Kaskazini yalivyokuwa yanaathiri raia.

Amesema kuwa hadi sasa, hakuna hatua zilizopigwa katika kuhakikisha kuwa watu walioathiriwa na mapigano wanapata hata usaidizi wa kimsingi zaidi wa kibinadamu.

Wakati huo huo, Bi Amis amesema kuwa shughuli za ukulima Sudan Kusini zimevurugwa na mapigano na kutotekelezwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano. Alipoulizwa kuhusu hofu yake kubwa zaidi kuhusu hali nchini humo, Bi Amos amesema:

“Nina hofu kubwa, kwa sababu mapigano yakiendelea, na makubaliano yaliyofikiwa baina pande zote mbili yakivunjwa kila siku, tutashuhudia kuzorota kwa haraka kwa hali ya usalama wa chakula, ambayo inaweza kusababisha janga la njaa.”

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter