Baraza la Usalama lalaani mashambulizi ya kigaidi Afghanistan

16 Julai 2014

Baraza la Usalama limelaani vikali leo shambulizi la kujitoa mhanga lililotokea tarehe 15 Julai, maeneo ya Paktika, nchini Afghanistan pamoja na mashambulizi yaliyotokea mjini Kabul, ambayo yalidaiwa na kundi la Wataliban. Mashambulizi hayo yamesababisha vifo vya wananchi wengi wakiwemo watoto.

Baraza la Usalama limepeleka rambirambi zake kwa familia za wahanga, raia na serikali ya Afghanistan. Aidha, limeeleza kutiwa wasiwasi na vitendo vya Wataliban, Al-Qaida na makundi megine ya kigaidi ambayo yanaweka hatarini raia wa Afghanistan, na pia shughuli za polisi, jeshi na misaada ya kibinadamu.

Wanachama wa baraza hilo wamerudia msimamo wao wa kupambana na kila aina ya ugaidi, chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa, wakiongeza kwamba hakuna tukio lolote la kigaidi linaloweza kuzuia raia na serikali ya Afghanistan kujenga amani na utulivu nchini humo.