Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Haki ya binadamu ya faragha ni lazima ilindwe popote

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa, Navi Pillay(Picha ya UM)

Haki ya binadamu ya faragha ni lazima ilindwe popote

Ufuatiliaji unaofanywa dhidi ya watu na serikali na kampuni kubwa za biashara bila idhini ya watu binafsi, ni ukiukwaji wa haki zao, ikiwemo haki ya kuwa na faragha, kwa mujibu wa ripoti mpya iliyochapishwa na Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa.

Taarifa kamili na Amina Hassan

Ripoti hiyo yenye kichwa, “haki ya faragha katika enzi za dijitali”, inasema kuwa kuna hali inayotia shaka ya kutokuwa na uwazi kuhusu sera na vitendo vya serikali kufuatilia watu, ikiwemo kulazimisha kampuni za sekta binafsi kuwezesha serikali kupata maelezo na takwimu kuhusu watu binafsi.

Ripoti inasema kuwa vidude vya kiteknolojia ambavyo sasa vinategemewa zaidi na watu katika maisha yao ya kisiasa, kiuchumi na kijamii, siyo tu vimo hatarini kuingiliwa, lakini pia vinawezesha serikali kupata maelezo ya watu ya faragha.

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa, Navi Pillay amesema kuwa nchi nyingi zinadakia udhaifu wa kutokuwepo sheria tosha na udhibiti wa uchunguliaji wa kidijitali kuendeleza mwenendo wa kukiuka haki ya kuwa na faragha.

Amependekeza kuwa ufuatiliaji wowote wa mawasiliano ya kidijitali ni lazima ufuatiliwe na kusimamiwa na taasisi huru.

 “Ufuatiliaji siyo jambo la kuchukuliwa hivi hivi tu. Unaweza kusababisha uharibifu au maangamizi. Katika baadhi ya nchi, watu wanaotambuliwa kama waasi wa serikali na ufuatiliaji wa dijitali wamelengwa kufanyiwa uchunguzi zaidi, na wakati mwingine, wameteswa au kudhulumiwa. Kukifanywa kwa kuzingatia sheria, na haki za binadamu, uchunguzi wa siri na mawasiliano ya dijitali unaweza bila shaka kuwa na ufanisi na umuhimu kwa ajili ya utekelezaji wa sheria. Kuwepo kwa ufuatiliaji kunatatiza kufurahia haki ya kuwa na faragha. Ni jukumu la serikali kuhakikisha kuwa uingiliaji huu wa faragha ya watu hautendwi kiholela au kinyume na sheria.”

Bi Pillay ameongeza kuwa kuwafuatilia watu kwa misingi ya rangi, dini au nchi wanakotoka hakutimizi kanuni za sheria za kimataifa, na kunaweza kuwa njia moja ya ubaguzi.