Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu milioni 19 kati ya milioni 35 hawajui kama wana virusi vya HIV:UNAIDS

Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS, Michel Sidibé,@UNAIDS

Watu milioni 19 kati ya milioni 35 hawajui kama wana virusi vya HIV:UNAIDS

Ripoti mpya ya Shirika linalohusika na HIV na Ukimwi, UNAIDS, imeonyesha kuwa takriban watu milioni 19 kati ya watu wapatao milioni 35 wanaoishi na virusi vya HIV kote duniani, hawajui kama wana virusi hivyo.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS, Michel Sidibé, juhudi zinapaswa kuongezwa kwa njia bora zaidi ili kuondoa tofauti baina ya watu wanaojua na wale wasiojua, wanaopata huduma na wasiopata, na baina ya wale wanaolindwa na wasiolindwa.

Taarifa kamili na George Njogopa

Ripoti hiyo inasema kuwa kadri watu wanavyojaribu kutambua hali zao za kiafya ndivyo hivyo hivyo watakavyojitahidi kupata matibabu kwa ajili ya kuokoa maisha yao.

Ripoti inabainisha kuwa katika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara karibu asilimia 90 ya watu ambao wamepima afya zao na kubaini kuwa wameambukizwa virusi vya HIV, wamekuwa wakipata madawa ya kufubaza makali ya virusi hivyo yaani ARV.

Katika ripoti hiyo UNAIDS imesema kuwa juhudi za usambazaji wa madawa ya kufubaza makali ya virusi hivyo imepata mafanikio na kwamba katika kipindi cha mwaka 2013, kiasi cha watu waliopata madawa hayo kiliongezeka kwa million 2.3. Kwa kuzingatia ripoti hiyo jumla ya watu wanapata madawa hayo sasa inakaribia kufikia milioni 13 duniani kote.

Michael Sidibe ni Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS.