Umoja wa Mataifa kuongeza vigezo vya biashara ya viungo vya pilipili

14 Julai 2014

Viungo kama pilipili manga, oregano ama majani ya chai vina hatari ya kuambukizwa na vidudu mbali mbali, kwa mujibu wa Kamati ya Umoja wa Mataifa inayohusu vigezo vya vyakula, Codex Alimentarius.  Majukumu ya Kamati hiyo ambayo imeundwa na Shirika la Chakula na Kilimo FAO na Shirika la Afya Duniani WHO ni kulinda afya ya watumiaji wa vyakula na kuendeleza tabia inayoheshimu sheria katika biashara za vyakula.

Ripoti iliyotolewa hivi karibuni imeonyesha kwamba viungo vingi vinapitia utaratibu mrefu wa kuvikausha, kuvisaga na kuvisafirisha ambapo viungo vinaweza kuambukizwa na vidudu kama salmonella, kemikali mbalimbali, mawe au vioo.

Katika mkutano unaofanyika wiki hii Geneva kwa ajili ya kuangalia vigezo vya usalama na ubora vya vyakula, Codex imeamua kuongeza vigezo vya kimataifa kuhusu kilimo cha viungo, usafi na afya ya wafanyakazi wa sekta hii, vifaa vinavyotumika, uwekaji na usafirishaji wao.

Vigezo vya kimataifa vya kwanza kabisa kuhusu biashara ya viungo vilianza kuwekwa mwanzo mwa mwaka huu tu, kutokana na ukuaji wa kasi wa sekta hiyo ya biashara.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter