Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama laazimia kuanzisha utaratibu wa ukaguzi wa misaada ya kibinadamu Syria

Kikao cha baraza la Usalma @NICA

Baraza la Usalama laazimia kuanzisha utaratibu wa ukaguzi wa misaada ya kibinadamu Syria

Wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo kwa kauli moja wamepitisha azimio la kuanzishwa kwa utaratibu wa ukaguzi wa shughuli za upakiaji, usafirishaji na upekuzi wa shehena zote za misaada ya kibinadamu ya Mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau wake kwa ajili ya raia wa Syria.

Akitangaza matokeo ya kura ya azimio hilo, Rais wa Baraza hilo ambaye pia ni Mwakilishi wa Kudumu wa Rwanda, Richard Gasana, amsema:

GASANA

“Matokeo ya kura ni kama ifuatavyo. Mswada umepata kura 15, na hivyo umepitishwa kwa kauli moja kama azimio namba 2165 (2014)”

Utaratibu huo ambao utakuwa chini ya mamlaka ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, pia utasimamia uvushaji wa shehena za misaada kuingia nchini Syria, kupitia vituo vya mpakani vya Bab al-Salam, Bab al-Hawa, Al Yarubiyah na Al-Ramtha, kwa kuzijulisha mamlaka za Syria ili kuhakikisha kuwa shehena hizo ni kwa ajili ya misaada ya kibinadamu.

Baraza la Usalama pia limesema pande zote katika mzozo wa Syria, hususan mamlaka za Syria, ni lazima zitimize wajibu wao chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu, na kutekeleza vipengele vya azimio lake namba 2139 la mwaka 2014, na taarifa za rais wa Baraza hilo ya tarehe 2, Oktoba 2013.

Baraza la Usalama pia limezitaka pande zote katika mzozo wa Syria kuwezesha mara moja ufikishaji wa misaada ya kibinadamu kwa watu wa Syria moja, bila vizuizi vyovyote, kulingana na tathmini ya Umoja wa Mataifa kuhusu mahitaji yao.

Taarifa ya azimio hilo pia imelaani vikali ukiukwaji ulioenea wa haki za binadamu na sheria ya kimataifa ya kibinadamu, ambao unatekelezwa na mamlaka za Syria na makundi yenye silaha.