Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Saudia Arabia yatoa taarifa kuhusu maambukizi ya kirusi corona

Hospitalini, Saudi Arabia @WHO

Saudia Arabia yatoa taarifa kuhusu maambukizi ya kirusi corona

Saudia Arabia imetoa taarifa kuelezea mwenendo wa maambukizi ya virusi vya corona ambavyo tayari vimeua watu kadhaa na wengine wakiendelea kupata matibabu.

Taarifa iliyotolewa na kitengo kilichowekwa maalumu kwa ajili ya kufuatilia hali ya ugonjwa huo imeonyesha kuwa kuanzia tarehe 3 Julai hadi tarehe 10 Julai, jumla ya wagonjwa 7 zaidi walithibitika kuambukizwa virusi vya homa ya corona, pamoja na kifo cha mtu mmoja aliyethibitishwa kuambukizwa awali.

Taarifa hiyo imesema mama mmoja kutoka eneo la Addawaser lililoko katika jimbo la Riyadh aligundulika kukumbwa na virusi hivyo baada ya vipimo vya maabara kuthibitisha. Pamoja na kwamba awali afya yake ilikuwa mbaya lakini sasa inasemekana anaendelea vizuri.

Mgonjwa mwingine aligundulika katika mji wa Jeddah katika jimbo la Makkah na hadi sasa anaendelea vyema na matibabu.

Mgonjwa wa mwisho aliyekumbwa na virusi hivyo ni kutoka katika mji wa Arar ambaye kwa bahati mbaya alifariki dunia Julai 6.

Kwa ujumla, kumekuwa na visa 834 vya homa ya corona vilivyothibitishwa kote duniani, huku watu wapatao 288 wakipoteza maisha kutokana na homa hiyo.