Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya nusu ya watu duniani sasa wanaishi mijini: UM

Mji wa Dhaka, Bangladesh Picha ya UM/Kibae Park

Zaidi ya nusu ya watu duniani sasa wanaishi mijini: UM

Asilimia 54 ya watu kote duniani sasa wanaishi mijini, na kiwango hicho kinatarajiwa kuongezeka hadi asilimia 66 ifikapo mwaka 2050. Hayo yamedhihirika katika ripoti mya ya makadirio ya Umoja wa Mataifa kuhusu ukuaji wa miji duniani, ambayo imezinduliwa leo mjini New York na idara ya masuala ya kiuchumi na kijamii ya Umoja wa Mataifa.

Makadirio hayo yanaonyesha kuwa ukuaji wa miji, pamoja na ukuaji wa idadi ya watu kwa ujumla unaweza kuchangia watu wengine bilioni 2.5 kuishi mijini ifikapo mwaka 2050, huku takriban asilimia 90 ya ongezeko hilo likiwa Asia na Afrika.

Makadirio hayo pia yanaonyesha kuwa ukuaji mkubwa zaidi wa miji utashuhudiwa India, China na Nigeria, ambazo kwa pamoja zinatarajiwa kuchangia asilimia 37 ya ukuaji wa idadi ya watu mijini kati ya mwaka 2014 na 2050.

Ifikapo mwaka 2050, idadi ya watu mijini India inatarajiwa kuongezeka kwa milioni 404, Uchina kwa milioni 292 na Nigeria kwa milioni 212.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, mji unaoongoza kwa idadi kubwa zaidi ya watu duniani ni Tokyo, yenye watu milioni 38, ukifuatiwa na Delhi, Shanghai, Mexico City, São Paulo na Mumbai.