Ripoti mpya yatolewa kuhusu kuzuia malaria na afya ya mama na watoto

10 Julai 2014

Ripoti mpya inayoonyesha faida za kupambana na malaria kwa afya ya akina mama na watoto imezinduliwa leo kwenye hafla maalum kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York.

Akizungumza na Redio ya Umoja wa Mataifa, daktari Erik Mouzin kutoka Ushirikiano wa Kutokomeza Malaria, ameeleza faida hizo akisema:

“ nadhani kwamba watu wamepata habari juu ya ufanisi uliopatikana katika vita dhidi ya malaria, lakini wachache wanajua kwamba wanawake wajawazito na watoto wadogo wenye umri chini ya mwaka mmoja, wameathirika sana na ugonjwa huo. Ni lazima kuchukua hatua kuzuia ugonjwa huo kwa watu hawa walio hatarini zaidi”.

Daktari Mouzin amesema, utafiti unaonyesha kwamba matumizi ya dawa maalum za kinga dhidi ya malaria wakati wa uja uzito na pia matumizi ya vyandarua vya kuzuia mbu yanaweza kupunguza hatari ya vifo kutokana na malaria katika siku za kwanza za uhai wa mtoto.

“ Tumeweza kupunguza idadi ya vifo vinavyosababishwa na malaria kutoka milioni 1 mwaka 2000 hadi 660 000 mwaka huu, hasa kwenye nchi za Rwanda, Senegal, Tanzania ama Zambia, ambapo hatua zilichukuliwa vizuri. Tumeonyesha pia kwamba tunaweza kuokoa maisha ya watoto wenye umri chini ya mwezi mmoja, kwa asilimia 18, kwa kutumia kinga. Ni Hatua nyingine gani rahisi kama hiyo inaweza kuleta mafanikio makubwa? Hakuna.”  

Amesema, zaidi ya asilimia 70 ya wanawake barani Afrika siku hizi wanapata fursa ya kuonana na daktari kabla ya kujifungua, tofauti na zamani, lakini bado kinga dhidi ya malaria haijapewa kipaumbele.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud