Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yahamishia wakimbizi wa Syria kwa kambi mpya nchini Iraq.

Wakimbizi kutoka Syria wakiingia mkoa wa Kurdistan nchini Iraq. Picha@UNHCR/G.Gubaeva

UNHCR yahamishia wakimbizi wa Syria kwa kambi mpya nchini Iraq.

Licha ya nchi ya Iraq kuwa na wakimbizi wa ndani kwa ajili ya mapigano katika nchi hiyo, Shirika la Kuhudumia Wakimbizi , UNHCR, linaendelea kusaidia wakimbizi kutoka Syria waliohamia Iraq baada ya machafuko nchini mwao.

UNHCR imefungua Kambi ya kudumu katika mkoa wa Kurdistan ulio kaskazini mwa Iraq, ili kuhudumia wakimbizi zaidi ya 225,000 kutoka Syria ambao walijiandikisha nchini Iraq kwa muda wa miaka miwili iliyopita. Wakimbizi 3,000 walioko kwa kambi ya hifadhi ya muda ilioko Arbat mjini Sulymaniah, wanahamishwa kwenda kwa kambi nyigine ambayo ina makazi bora zaidi kaskazini mwa nchi hiyo. Hata hivyo, wakimbizi wengi wanaoingia Iraq wamejitafutia makao ya kibinafsi, na inatarajiwa kuwa idadi ya wakimbizi katika sehemu hiyo itafikia zaidi ya 10,000.

Afisa wa UNHCR mjini Sulyaminah, Bwana Kahin Ismail amesema kwamba kambi hiyo imejengwa kwa wakati ambapo raia wengi wa Syria wanatoroka kwao na kusaka hifadhi, na akaongeza kusema kuwa wanataraji wakimbizi wengi watahamia kambi hiyo kutoka kwa miji mbali mbali, pamoja na sehemu nyingine za nchi hiyo hasa wakati watakapokabiliwa na upungufu wa pesa za kujikimu mijini.

Bwana Kahin ameendelea kusema kuwa, kulingana na hali mbaya inayoendelea nchini Syria, wakimibizi hao wataishi kwa kambi hizo kwa muda mrefu.

Wakimbizi waliohamishwa wameonyesha furaha yao kwa makazi yaliyoko kwenye kambi hiyo mpya ambayo ina zahanati ya huduma za afya na shule kwa watoto, pamoja na maduka yenye bidhaa za mahitaji yao muhimu.