WHO yaihimiza Uchina kuendelea kufanyia marekebisho mfumo wake wa afya

9 Julai 2014

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, WHO, Dr. Margaret Chan, amesema ni jambo la umuhimu mkubwa kwa serikali ya Uchina kuendelea na hata kuongeza kasi ya kufanyia marekebisho mfumo wake wa huduma za afya, ili kujenga mfumo utakaokabiliana na changamoto za afya sasa na za siku zijazo.

Dr. Chan amesema hayo wakati akikamilisha ziara yake rasmi nchini Uchina, akisema serikali ya Uchina imepiga hatua kubwa katika kurekebisha mfumo wa afya katika miaka ya hivi karibuni, kwani sasa asilimia 95 ya raia wote wa nchi hiyo wana bima ya afya na watu sasa wanapata huduma za afya kuliko ilivyokuwa zamani.

Uzingativu wa serikali ya Uchina katika kufanyia marekebisho mfumo wake wa afya umeungwa mkono kwa uwekezaji wa kimo kikubwa na endelevu, kwani matumizi ya fedha za serikali katika sekta ya afya yaliongezeka maradufu katika kipindi cha mwongo mmoja.

Licha ya ufanisi huo, Dkt. Chan amesema hatua zaidi zinatakiwa pamoja na uwekezaji zaidi, hususan katika kupanua wigo wa huduma za afya ya kimsingi na jamii, na kuboresha ushirikiano wa huduma za kimsingi na hospitali ili kuwe na huduma zinazowajali wagonjwa zaidi.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter