Jamii za wavuvi ziwa Tanganyika zabadilisha mbinu za kukausha samaki

9 Julai 2014

Shirika la Chakula na Kilimo Duniani, FAO, limetoa ripoti mpya kuhusu mafanikio ya mradi lililoutekeleza katika jamii za wavuvi wa samaki ndogondogo, ziwani Tanganyika, nchini Burundi.  Samaki hao wanaoitwa ndagala, kawaida hukaushwa chini.  Mchanga, mvua na matope huharibu bidhaa hizo mara kwa mara, jinsi anavyoeleza afisa wa FAO Yvette Diei Ouadi:

“ Ilikadiriwa, mwaka 2004, kwamba asilimia 15 ya samaki waliokamatwa walikuwa wanapotea au wanaharibika wakati wa kuwakausha. Uharibifu huo ulikuwa unawakumba wadau wote wa biashara hiyo”

Shirika la Fao limesaidia wavuvi wa kijiji kimoja kutengeneza chanja za kukausha, zilizo juu kidogo na zenye kifuniko ili kuzuia mvua. Baada ya muda mfupi, vijiji vingine vilianza kuiga mfano wa kijiji hicho.

“Uvumbuzi huo umeimarisha usafi na usalama wa bidhaa yenyewe. Bei ya bidhaa imepanda na imeongeza kipato cha wavuvi na wadau waote wa biashara hiyo. Bei imepanda kutoka dola mbili na nusu kilo hadi dola sita kwa kilo. Mabadiliko ni makubwa kwa jamii.”

Yvette amesema, shirika la FAO limeridhishwa sana na mradi huo ambao ni endelevu na umesaidia kutunza rasilimali za ziwa Tanganyika.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter