Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanawake 145,000 wakimbizi wa Syria wanaubeba mzigo wa familia zao: UNHCR

Mstari wa wanawake wakikimbia Syria, wakibeba watoto, wakivuka ndani ya Jordan kutoka kusini mwa Syria. Picha: UNHCR/N. Daoud.

Wanawake 145,000 wakimbizi wa Syria wanaubeba mzigo wa familia zao: UNHCR

Ripoti mpya ya Shirika la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, imesema zaidi ya familia 145,000 za wakimbizi wa Syria zilizoko Misri, Lebanon, Iraq na Jordan, au kila moja katika familia zote za wakimbizi, zinaongozwa na wanawake ambao wanahangaika peke yao kujikimu kimaisha.

Ripoti hiyo inaweka bayana mahangaiko ya kila siku ya kutafuta riziki, huku wanawake hao wakijitahidi kuendeleza utu wao na pia kulea familia zao katika makazi duni yenye watu wengi na mahema ya muda yasiyo salama. Wengi wao wanakabiliwa na tishio la ukatili na unyanyasaji, huku watoto wao wakikabiliwa na madhila na machungu yanayoongezeka kila uchao.

Ripoti hiyo iliyopewa kichwa, “Mwanamke pweke- mahanagiko ya kuishi kwa wanawake wa Syria wakimbizi”, imetokana na maelezo binafsi ya wanawake 135, ambayo yametolewa kwa kipindi cha miezi mitatu ya mahojiano mwaka 2014.

Wakiwa wamelazimika kuchukua majukumu ya kulea familia zao baada ya waume zao kuuawa, kutekwa au kutenganishwa na vita, wanawake hao wamejikuta kwenye wimbi la mahangaiko na hofu. Tatizo la kwanza wanaloripoti wanawake hao ni ukosefu wa rasilmali, huku wengi wao wakihangaika kulipa kodi ya nyumba, kukidhi mahitaji ya chakula na kununua bidhaa za nyumbani.

UNHCR imetoa wito hatua mpya za dharura zichukuliwe na wafadhili, nchi zinazowapa hifadhi na mashirika ya misaada ya kibinadamu ili kuwasaidia wanawake hao.