Tatizo la Ebola Afrika Magharibi lapatiwa sikio kwenye Baraza la Usalama

8 Julai 2014

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo limesikiliza ripoti ya Katibu Mkuu kuhusu ukanda wa Afrika ya Magharibi, ikitaja hali tete eneo la Sahel na kuzorota usalama nchini Nigeria, huku suala la Ebola likitajwa kama linalopaswa kupewa kipaumbele na jamii ya kimataifa.

Taarifa ya Joshua

Baraza hilo ambalo limekutana kuhusu uimarishaji amani Magharibi mwa Afrika, limehutubiwa na Mwakilishi Maalumu wa Katibu Mkuu kuhusu ukanda wa afrika Magharibi, Said Djinit, ambaye amesema kutokana na hali tete iliyotanda ukanda huo, juhudi zote zinatakiwa kufanywa kuhakikisha kuwa demokrasia na utulivu vinatafutwa kwa nguvu sawa kwani viwili hivyo vinashabihiana.

Bwana Djinit amesema hali ukanda wa Sahel bado ni ya kutia wasiwasi kwa sababu ya aina nyingi za udhoofu katika utawala, usalama, mazingira na maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Amesema kuna haja ya kuweka uataratibu wa pamoja kwa ajili ya Sahel.

Djinit amezungumza pia kuhusu hali nchini Nigeria ambayo bado ni tete, huku ukatili dhidi ya raia ukiendelea kutekelezwa na Boko Haram.

Hatimaye Djinit amezungumzia tatizo la ugonjwa wa Ebola, unaoendelea kusambaa kwenye eneo hilo

“Kumekuwa na maambukizi yapatayo 759 na vifo 467 vinavyohusishwa na ugonjwa huu. Ni muhimu jamii ya kimataifa kuzingatia na kusaidia kukabiliana na ugonjwa huu ambao unaongeza matatizo mengine mengi, yakiwemo ya utulivu katika eneo hilo.”

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter