Idadi ya wahamiaji wanaokufa Mediterenia yaendelea kuongezeka
Idadi ya wahamiaji ambao wamekufa kwenye Bahari ya Mediterenia wakijaribu kukimbilia Ulaya imeongezeka na kufikia watu 500, kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR.
Mnamo Jumatatu, walinzi wa pwani ya Libya waliiambia UNHCR kuwa walikuwa wametoa miili 12 kutoka kwenye ajali ya boti ambayo inaaminika kutokea Jumapili. Miongoni mwa wahanga alikuwemo mama mmoja kutoka Syria na wanawe wawili wenye umri wa miaka mitatu na sita.
UNHCR imesema boti hiyo ilikuwa imejazwa kupindukia, ikiwa imezidi uwezo wake wa kubeba watu 200. Takriban waomba hifadhi na wakimbizi 37,000 wameandikishwa na maafisa wa UNHCR Tripoli na Benghazi, wengi wao wakiwa ni Wasyria.