Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Malengo ya Maendeleo ya Milenia yanaleta mabadiliko: Ban

UN Photo/Paulo Filgueiras
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon. Picha@

Malengo ya Maendeleo ya Milenia yanaleta mabadiliko: Ban

Wakati dunia ikiangazia awamu ya mwisho ya harakati za kufikia malengo ya maendeleo ya milenia, MDGs, ni dhahiri sasa kuwa malengo hayo yanaleta mabadiliko katika maisha ya watu. Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, wakati wa kikao cha Baraza la masuala ya Kiuchumi na Kijamii, ambapo pia imezinduliwa ripoti ya hatua zilizopigwa katika safari ya kuyafikia malengo hayo. Taarifa kamili na Amina Hassan

Ban amesema kuwa malengo ya maendeleo ya milenia yamesaidia kuleta umoja, kutoa msukumo na kuleta mabadiliko. Amesema kufikia sasa, malengo mengi muhimu yametimizwa au yamo mbioni kufikiwa.

Ametaja baadhi ya malengo yaliyotimizwa kama vile kupunguza idadi ya watu wanaoishi katika umaskini uliokithiri kwa asilimia hamsini, na ile ya watu wasiopata maji safi, miaka mitano kabla ya tarehe ya ukomo mwakani.

“Ufanisi mkubwa umepatikana katika vita dhidi ya malaria na kifua kikuu, vifo kutokana na malaria vikipunguzwa kwa asilimia 42 kote duniani. Utofauti wa kwenda shule kati ya wavulana na wasichana umepunguzwa. Malengo mengine muhimu kama upatikanaji wa dawa za kupunguza makali ya HIV, na utokomezaji wa kemikali zinazoharibu eneo la ozoni karibu yatatimia.”

Ban amesema, ufanisi huu unaonyesha kuwa hatua za pamoja za serikali, jamii ya kimataifa, mashirika ya umma na sekta ya kibinafsi zinaweza kuleta mabadiliko. Hata hivyo, amesema kuwa ufanisi huo haujawa kwa kiwango cha usawa kwa maeneo na nchi zote, na pia katika jamii mbali mbali.