Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pillay akemea ubaguzi wa elimu dhidi ya watoto wa kike, wanawake

Pillay akemea ubaguzi wa elimu dhidi ya watoto wa kike, wanawake

Pamoja na wito unaoendelea kutolewa na jumuiya za kimataifa unaotaka kuondolewa kwa aina yoyote ya ubaguzi dhidi ya wanawake ikiwemo haki ya kupata fursa, lakini hadi sasa inakadiriwa kuwa zaidi ya watoto wa kike milioni 35 wameshindwa kupata elimu wanayostahili. Taarifa kamili na John Ronoh

Kulingana na Kamishna wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Navi Pillay, kuwepo kwa mkusanyiko wa mambo kama vile mifumo dume, mila potufu kumesababisha watoto wengi wa kike na wanawake kwa ujumla kunyimwa haki zao za msingi za kupata elimu.

Akizungumza kwenye mkutano kuhusu haki ya kupata elimu kwa wanawake na watoto wa kike uliondaliwa na Kamati Maalumu ya Umoja wa Mataifa inayohusiana na upigaji vita vitendo vyote vya ubaguzi dhidi ya wanawake(CEDAW) Bi Pillay amesema kuwa kushindwa kubaini kasoro hiyo ya kuwabagua wanawake kupata elimu kumesabisha kuwepo kwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

Hata hivyo amesema kuwa dunia inapaswa kuhakikisha kwamba inaendelea kutoa msukumu ili kuwawezesha watoto wote wa kike kupata fursa ya kupata elimu. Amesema kuwa watoto wa kike ni sawa kama walivyo watoto wa kiume hivyo hakuna sababu ya kuwanyima fursa ya kusoma.