Kuwazuilia watafuta hifadhi na wakimbizi kukomeshwe: UNHCR

3 Julai 2014

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, leo limetoa mkakati wa kimataifa unaolenga kuzisaidia nchi kukomesha desturi ya kuwakamata na kuwazuilia watafuta hifadhi, wakimbizi na watu wasio na utaifa kote duniani. Taarifa kamili na Joshua Mmali

Taarifa ya Joshua

UNHCR imesema kuwa desturi hiyo katika baadhi ya nchi ina madhara makubwa na ya muda mrefu kwa watu wahusika na familia zao, huku ikieleza kusikitishwa na kuenea kwa uzuiliaji wa watu na idara za uhamiaji, hususan watoto.

Mkakati huo mpya wa UNHCR uitwao, Hatua Inayozidi Uzuiliaji, unatoa wito kwanza ukomeshwe uzuiliaji watoto, pili, kuhakikisha kuwa kuna hatua mbadala zinazochukuliwa kisheria, na tatu kuhakikisha kuwa mazingira ya uzuiliaji, pale usipoepukika, yanatimiza viwango vya kimataifa vya haki za binadamu.

Volker Türk ambaye ni Mkurugenzi wa Ulinzi wa Kimataifa katika UNHCR, amesema kuwa kutafuta hifadhi ni kitendo halali na cha haki kwa binadamu, na kwamba watu wanaotafuta hifadhi wapewe ulinzi badala ya kuzuiliwa.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud