Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO, Ulaya yaweka mkakati mpya kukabili kifua kikuu

Wagonjwa wa kifua kikuu kutoka Myanmar wakiishi kwenye vibanda wakati wa matibabu katika Klinik ya Wangpha kwenye mpaka wa Thailand. Picha: IRIN/Sean Kimmons(UN News Centre)

WHO, Ulaya yaweka mkakati mpya kukabili kifua kikuu

Shirika la afya ulimwenguni WHO kwa kushirikiana na chama cha upumiaji barani Ulaya, leo kimetoa mwongozo mpya unaoainisha mikakati ya kukabiliana na tatizo la ugonjwa wa kifua kikuu katika nchi ambazo tatizohiloni la kiwango cha chini.

Hadi sasa inaelezwa kuwa kuna nchi 33 duniani ambazo kiwango cha ugonjwa huo kipo chini na kwamba kila kwenye idadi ya watu milioni basi kuna matukio chini ya 100 ya kifua kikuu.

Taarifa zaidi na George Njogopa

Mpango huo uliotolewa unaonyesha hatua za kwanza zinazopaswa kuchukuliwa ili kuhakikisha kwamba kiwango cha ugonjwa huo  katika nchi hizo kinapungua kabisa ifikapo mwaka 2035.

Mpango huo unaonyesha kwamba katika awamu ya kwanza kiwango hicho kinapaswa kupungua kutoka kile cha sasa. Mapendekezo yaliyopo ni kwamba kila kwenye idadi ya watu milioni basi kuwepo kwa matukio ya watu wanaosumbiliwa na ugonjwa wa kifua kikuu yasiyozidi 10.

Kufanikiwa kwa mpango huo kutasaidia kufikia shabaha iliyowekwa kimataifa inayotaka ifikapo mwaka 2050 tatizo la kifua kikuu liwe limetoweka kabisa.

Ripoti zinaonyesha kwamba tatizo la kifua kikuu limekuwa likiziandama nchi nyingi duniani na kwamba katika nchi hizo 33 zilizoelezwa, inaelezwa kwamba kila mwaka watu 155,000 hupatwa na ugonjwa huo na kati ya hao 10,000 hupoteza maisha. Mamilioni ya wengine wameathiriwa na ugonjwa huo na wakati wowote wapo hatarini kuugua ugonjwa huo.

Baadhi ya mikakati iliyopendekezwa ili kutokomeza tatizohiloni pamoja na kuhakikisha kwamba kunawepo mafungu ya fedha kwa ajili ya kutoa huduma bora dhidi ya tatizohilo. Pia kutoa vipimo vya mara kwa mara na kutoa vipaumbele kwenye maeneo ambayo yanaonekana kuwa hatarini kukubwa na tatizo hilo.