Mwakilishi wa UM Somalia alaani mauaji ya mbunge "Hayd"

3 Julai 2014

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, Nicholas Kay, amelaani vikali mauaji ya mbunge Mohamed Mohamud “Hayd” na mlinzi wake yaliyotokea leo asubuhi mjini Mogadishu, akieleza kutiwa wasiwasi na mashambulizi kadhaa yanayodaiwa na kundi la Al-Shabab tangu mwanzo mwa Ramadan.

Nicholas Kay amesema, mwezi wa Ramadan ni mwezi wa amani na maridhiano, na kuuawa watu wakati wa mwezi huu ni dalili ya kuwa watekelezaji hawa hawajali maisha ya Wasomali.

Mwakilishi huyu ameiomba serikali ya Somalia iwapeleke waliotenda mauaji hayo mbele ya sheria haraka iwezekanavyo, akisisitiza msimamo wa Umoja wa Mataifa kuziunga mkono juhudi za wananchi na wawakilishi wa Somalia ili kuleta amani ya kudumu nchini.

Hatimaye, amepeleka rambirambi zake kwa familia za wahanga na Bunge la Somalia.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter