Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rwanda kuongoza Baraza la Usalama Julai, ulinzi wa amani kuwekwa mbele

Rwanda kuongoza Baraza la Usalama Julai, ulinzi wa amani kuwekwa mbele

Rwanda itaongoza Baraza la Usalama kwa kipindi cha mwezi mzima wa Julai. Mwakilishi wa kudumu wa nchi hiyo, Eugene Gasana, amesema kwamba urais huo utazingatia Ulinzi wa Amani, Rwanda ikiadhimisha mwaka huu miaka kumi tangu ilipoanza kuchangia katika jeshi la Ulinzi wa Amani la Umoja wa Mataifa.

Katika muktadha huo, Rwanda imeamua kuandaa mjadala wa mawaziri wa ukanda wa Afrika ya Mashiriki na bara la Afrika zima kuhusu ushirikiano wa kikanda ili kuendeleza ulinzi wa amani. Azimio linatarajiwa kupitishwa kuhusu mada hiyo.

Waziri Gasana amewakumbusha waandishi wa habari pia kwamba Rwanda itaadhimisha tarehe 4, Julai, miaka ishirini ya ukombozi wan chi hiyo baada ya mauaji ya kimbari.

Mijadala mingine inayotarajiwa kujitokeza mwezi huu ni kuhusu Afrika ya Magharibi, Sudan Kusini, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Syria, na kadhalika. Akijibu swali kutoka waandishi wa habari kuhusu hatua zinazochukuliwa na MONUSCO kupambana na FDLR, amesema Rwanda inataka kuona utashi kutoka MONUSCO:

“ Kila mtu anajua kwamba FDLR ni kikundi cha wauaji wa kimbari, na kimewekewa vikwazo na Umoja wa Mataifa. Sasa ni miaka 15 tangu MONUSCO ilipopelekwa DRC. Tunaka kuona matokeo sasa. Lakini, tunajua MONUSCO ni ujumbe mkubwa zaidi wa Umoja wa Mataifa lakini mpaka sasa hivi haitekelezi vyema kazi. Inapaswa kutekeleza operesheni zake ipasavyo lakini haifanyi.”