Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO, WHO yatoa orodha vyakula 10 vinavyoandamwa na wadudu

@FAO

FAO, WHO yatoa orodha vyakula 10 vinavyoandamwa na wadudu

Kumetolewa ripoti mpya inayoonyesha vyakula aina kumi duniani ambavyo ndani yake kunakutikana wadudu hatari wanaoweza kusababisha madhara makubwa kwa afya ya binadamu. Hata hivyo habari njema ni kwamba ripoti hiyo imebainisha mbinu za kukabiliana na wadudu hao wanaokaa ndani ya mimea.Taarifa zaidi na George Njogopa

Taarifa ya George

Imefahamika kuwa wadudu hao ambao wengi wao wanauwezo wa kuishi katika mwili wa binadamu kwa kipindi cha miongo kadhaa, wanatajwa kuwa na athari kubwa kwa afya na kwamba zaidi ya watu milioni moja huathirika kila mwaka.

Ripoti zinasema kuwa baadhi ya maeneo ambayo yanaathiriwa na wadudu hao ni pamoja na maeneo ya misuli hatua ambayo inaweza kusabisha ugonjwa wa kifafa. Pia mtu anapokumbwa na wadudu hao anaweza kukumbwa na ugonjwa wa kuhara damu.

Kwa mujibu wa ripoti zilizotolewa na mashirika ya Umoja wa Mataifa, lile la Chakula na Kilimo FAO na Shirika la Afya Ulimwenguni WHO, pamoja na kwamba tatizo hilo ni kubwa na limeendelea kusababisha hasara kubwa kwa maisha ya binadam lakini jambo la kushangaza ni kwamba taarifa zinazohusu wadudu hao bado ni chache.

Mashirika hayo yamesema kuwa bado wananchi hawajafikiwa kikamilifu na taarifa kamili kuhusiana na sehemu wanakotoka wadudu hao, jinsi wanavyoishi katika mwili wa binadamu na jambo kubwa zaidi namna wanavyoweza kuathiri afya za binadamu.

Katika hatua ya kukabiliana na tatizo hilo, mashirika hayo yamebainisha hatua zinazopaswa kuchukuliwa ikiwamo unyunyiziaji wa magadi maalumu kwa vyakula aina ya nyama na mboga mboga ili kuua wadudu jamii ya minyoo. Pia imependekeza utiwaji wa dawa zinazotambulika kitaaluma kwa vinywaji kama vile juisi na vyakula vingine.