Hilde Johnson aaga UNMISS , asema amani inahitajika kwa wakimbizi

30 Juni 2014

Mwezi wa Julai, tarehe 9, mwaka huu, nchi ya Sudan Kusini itaadhimisha miaka mitatu ya uhuru wake, na wakati uo huo, mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Hilde Johnson, ataondoka nchini humo, akiwa ametimiza miaka mitatu kama mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini, UNMISS.

Alipozungumza na waandishi wa habari leo mjini New York, Hilde Johnson amesema atakayechukua nafasi yake atakua na jukumu la kuhakikisha kwamba pande zote za mzozo wa Sudan Kusini zinatimiza ahadi zilizochukuliwa mwezi uliopita mbele ya viongozi wa IGAD, ikiwa ni kuandaa serikali jumuishi ya mpito ifikapo tarehe 10 mwezi Agosti. Amesema kinachohitajika:

“ vitu viwili vinapaswa kutekelezwa ifikapo tarehe 10, Agosti : kwanza, kusitisha kabisa mapigano, na pili, kuandaa hii serikali ya mpito. Kwa hiyo muda ni mfupi sana, na katika kipindi hicho cha mwezi moja, ni lazima kuona shinikizo la kimataifa ili pande zote ziheshimu makubaliano hayo na ziamue kuweka hatma ya nchi yao na raia wao mbele ya mambo yao ya kibinafsi.”

Halikadhalika, amesema amani inahitajika hasa kwa ajili ya wakimbizi wa ndani zaidi ya milioni1.5 ambao wanakumbwa na hatari ya ukosefu wa chakula. Hali yao hivi sasa ni mbaya zaidi kwa sababu ya msimu wa mvua, ameongeza, na Umoja wa Mataifa pamoja na mashirika ya kibinadamu zinajitahidi kuboresha hali ya maisha ndani ya kambi zao.

Hatimaye, alitoa ushauri wake kwa mwelekeo wa mzozo huo, akisema kwamba maridhiano yatahitaji uwajibikaji kamilifu kuhushu ukiukwaji wa haki za binadamu ulioshuhudiwa wakati wa mzozo.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud