Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Huduma za umeme na maji zimetatizika Aleppo, Syria: OCHA

Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephen Dujarric.(Picha UM/Maktaba)

Huduma za umeme na maji zimetatizika Aleppo, Syria: OCHA

Ofisi ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu, OCHA, imesema imepokea ripoti kuwa baadhi ya maeneo ya mji wa Aleppo nchini Syria hazina huduma za umeme kabisa, huku mengine yakiwa na umeme kwa chini ya saa moja kila siku.

Katika mkutano na waandishi wa habari mjini New York, msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric ameseme kuwa OCHA imesema huduma za maji pia zimekatizwa kwa zaidi ya siku kumi maeneo mengi ya mji huo wa Aleppo, huku baadhi ya maeneo yakipata maji mara moja tu kwa kipindi cha saa 5, kila baada ya siku tano.

“Shirika la Halali Nyekundu la Syria linaendelea kujaribu kufika vijijini Aleppo, ili kukarabati mabomba ya maji, nyaya za stima, ambazo zimeharibiwa katika mashambulizi tangu tarehe 2 Juni, ambayo yamewaacha watu wapatao milioni moja katika mji wa Aleppo bila huduma za maji.”

Bwana Dujarric amesema mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau wengine wanaendelea kutoa misaada ili watu milioni 16.5 waweze kupata maji safi na dawa za kutakatisha maji katika majimbo 14 ya Syria, na pia wahudumu wa kibinadamu karibuni wapetoa dawa kwa watu zaidi ya 138,000 Aleppo, pamoja na vifaa vya kupima usafi wa maji.

“Mratibu wa kibinadamu anaongoza mkakati wa kukabiliana na hali hii unaolenga kuzuia, kupima na hatua za kujiandaa kwa mkurupuko wa magonjwa ili kuhakikisha kuna maji safi ya kutosha na huduma za kujisafi katika maeneo ya hatari, kama vile maeneo wanapokaa wakimbizi wa ndani katika makazi ya halaiki.”