Wanasiasa ni lazima waondoe kutoaminika kwa mustakhabali wa demokrasia: IPU

30 Juni 2014

Wakati Shirika la Muungano wa Wabunge Duniani, IPU, likiadhimisha miaka 125 tangu kuundwa kwake, wanasiasa wametakiwa kuondoa ukosefu wa imani nao na kutumia mbinu jumuishi zaidi za kisiasa iwapo demokraisia itatakiwa kunawiri kama inavyotakiwa katika siku zijazo. Amina Haasan na taarifa kamili

Taarifa ya Amina

Shirika la IPU, ambalo ndilo shirika zee zaidi la kisiasa duniani linaloshirikisha nchi nyingi, lilianzishwa na kundi la wabunge wenye mtazamo wa kipekee wa kuwa na ulimwengu mpya wenye amani zaidi mnamo tarehe 30 Juni mnamo mwaka 1889, limewataka wabunge kote duniani kuwa mstari wa mbele katika kuleta mabadiliko.

Katika hafla ya maadhimisho ya karne moja na robo tangu lianzishwe, Rais wa IPU, Abdelwahad Radi, amesema kuwa demokrasia hukumbana na changamoto mpya kila uchao, na kwamba raia wanapokata tamaa na kukosa imani katika siasa za kijadim, hali hiyo inaongeza unyanyasaji wa makundi ya pembezoni na hivyo kudhoofisha demokrasia.

Katika hafla hiyo, Kinara wa zamani wa bunge la Kenya, Kenneth Marende, amezungumzia funzo lililotokana na machafuko baada ya uchaguzi Kenya mwaka 2007

“Amani haiwezi kuchukuliwa hivi hivi tu. Ni lazima tufanye juhudi kila siku ili kuilinda ili tuweze kuiendeleza na pia kuendeleza utawala wa demokrasia.”

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud