Ban asikitishwa na hali inayozidi kuzorota Iraq, ahimiza ulinzi wa raia

30 Juni 2014

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, ameelezea kutiwa hofu na hali inayozidi kuzorota nchini Iraq, na idadi inayoongezeka ya raia wanaouawa na kujeruhiwa, huku watu milioni moja wakiwa wamelazimika kuhama makwao kwa sababu ya mapigano.

Taarifa iliyotolewa na msemaji wake imesema kuwa Ban ametoa wito kwa pande zote katika mzozo huo kuhakikisha kuwa mateso ya raia kwa misingi ya kidini au kabila yanakomeshwa mara moja. Amesema pande zote hizo, iwe ISIL, wanamgambo wa ndani au jeshi la kitaifa la Iraq, zina wajibu wa kufanya lolote ziwezalo kuhakikisha raia hawalengwi katika mapigano hayo, na kuhakikisha kuwa mahitaji yao ya kibinadamu yanakidhiwa.

Katibu Mkuu pia ameelezwa kusikitishwa mno na ripoti za ukiukwaji wa haki za binadamu na sheria ya kimataifa ya kibinadamu ambao unaendelea nchini Iraq, ukiwemo mauaji ya wanajeshi waliokamatwa na wafungwa, pamoja na kushambulia kwa makombora maeneo yanayokaliwa na raia, utekaji nyara na mauaji ya jamii za kidini na makabila fulani.

Ban ameitaka serikali ya Iraq pia iwawajibishe wanajeshi wa vikosi vya serikali au makundi ya wanamgambo ambao wamekiuka sheria ya kimataifa ya kibinadamu na haki za binadamu.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud