Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wa Sudan wasisahaulike: UNICEF

© UNICEF Sudan Kusini/2014/Pires
Watoto wakimbizi wa Sudan Kusini wakihudumiwa na maafisa wa misaada ya kibinadamu.

Watoto wa Sudan wasisahaulike: UNICEF

Wananchi wa Sudan hususan watoto, wanahitaji msaada wa kibinadamu kwa haraka, amesema Geert Cappelaere, mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF, nchini humo akizungumza katika mahojiano maalum na Redio ya Umoja wa Mataifa.

Amesema mzozo wa Sudan ni mbaya zaidi duniani kwa hali ya watoto kwa sababu tatu, mosi watoto ni wahanga wa dharura zitokanazo na mizozo iliyomo ndani ya nchi na katika nchi jirani.

Sababu ya pili, bado mizozo ya zamani kama ule wa Darfour ulioibuka miaka 10 iliyopita unaathiri watoto ambapo zaidi ya watu milioni 1.2 bado ni wakimbizi maeneo ya Darfur, asilimia 65 wakiwa watoto wenye umri chini ya miaka 18.

Bwana Geert ametaja sababu ya tatu kuwa ni upungufu wa uwekezaji pesa kutoka serikalini katika sekta za ustawi wa jamii ambao husababisha watoto wengi kutopata huduma za msingi kama vile afya na elimu, ambazo ni haki zao.

Mwakilishi huyo wa UNICEF amesema wanaajitahidi kutekeleza miradi mbali mbali ili kuboresha hudhuma hizo, akisema mpaka sasa wameweza  kufikia asilimiam 95 ya watoto.

Ingawa mwelekeo wa nchi si mzuri kwa upande wa uchumi na kisiasa, Bwana Geert ana matumaini akiona jinsi jamii na wazazi wanajitolea kuimarisha hali ya watoto wao, akitaja mfano ya kampeni ya kijamii dhidi ya ukeketaji wasichana.

“ Tumefikia karibia watoto wote, na bado tunajituma ili tuwafikie wote. Lakini ili tuwafikie inabidi pande zote wakubali kwamba ni lazima vita viishe. Naangalia sana hali ya uchumi, kisiasa ambayo si nzuri, lakini fursa zipo nyingi na muda umefika tuchukue fursa hizo kuwekeza leo katika Sudan. Na tuwekeze leo, si kesho”