Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vifo vya waja wazito vinaweza kuzuiwa: Ban

Ban akiwa na picha ya mwana wa simba Picha @Eskinder Debebe/UM

Vifo vya waja wazito vinaweza kuzuiwa: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, amesema kuwa ingawa hatua zimepigwa katika miaka ya hivi karibuni kupunguza vifo vya waja wazito, bado wanawake wengi sana wanafariki dunia wakati wa kujifungua mimba, au kutokana na matatizo yanayohusiana na mimba.

Ban amesema hayo katika hafla iliyoandaliwa na mke wa rais wa Kenya, Margaret Kenyatta ya kampeni inayokwenda hatua zaidi, ambako amesema kuwa vifo vingi vya waja wazito vinaweza kuzuiwa, na ndio maana ulizinduliwa mkakati wa Kila Mama Kila Mtoto.

Katibu Mkuu amehimiza uwekezaji katika masuluhu madogo madogo, kama vile mafunzo ya wakunga vijijini au pikipiki za usafiri wa dharura za kuwasaidia akina mama waja wazito katika maeneo magumu kufikiwa vijijini, akisema kuwa hakuna mwanamke hata mmoja anayestahili kufa wakati akijifungua mimba.

Akiwa Nairobi pia, Ban ametembelea hifadhi ya wanyama wa pori, ambako amechukua jukumu la kumlea mwana wa simba.