UNEA yataka hatua zichukuliwe kuzuia Vifo milioni 7 vitokanavyo na hewa chafu

28 Juni 2014

Kikao cha kwanza cha Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa, kimehitimishwa kwa wito wa kutaka hatua zichukuliwe ili kuboresha usafi wa hewa na kuzuia vifo milioni 7 vya mapema ambavyo hutokana na hewa chafu.

Kikao hicho cha siku tano kilihitimishwa pia kwa kupitisha maazimio 16 yanayohimiza hatua za kimataifa katika kukabiliana na masuala kadhaa yanayohusu mazingira, yakiwemo biashara haramu ya viumbe wa porini, usafi wa hewa, taka za plastiki katika mabahari, kemikali na taka kwa ujumla.

Akizungumza wakati wa kufunga kikao hicho, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, amesema kuwa hewa tunayopumua, maji tunayoyanywa na udongo tunamozalishia chakula, ni sehemu ya bayo anuai ambayo inaendelea kukabiliwa na shinikizo kubwa.

Baraza hilo lilitambulisha uchafuzi wa hewa kama tatizo linalopaswa kupewa kipaumbele na jamii ya kimataifa, ili kuepusha vifo milioni 7 kila mwaka, kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani, WHO.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter