Majanga mengi duniani ni ‘Mkono wa binadamu’: Ban

27 Juni 2014

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amesema Baraza la Mazingira la Umoja huo UNEA pamoja na shirika lake la mazingira UNEP yana dhima kubwa sasa kwenye mustakhbali wa maendeleo endelevu wakati malengo ya milenia yanapofiki ukomo mwakani.

Akizungumza mwishoni mwa baraza hilo mjini Nairobi, Kenya Ban amesema hewa ambayo binadamu wanavuta, maji wanayokunywa na udongo ambamo kwao wanapanda vyakula ni sehemu ya mfumo wa kiekolojia duniani ambao unazidi kuwa hatarini kutokana na shughuli za binadamu. Kwa mantiki hiyo Ban amesema ..

(Sauti ya Ban)

Kadri idadi ya watu inavyoongezeka, tunapaswa kutambua kuwa matumizi yetu ya rasilimali zilizopo duniani si endelevu. Tunaona visababishi vya binadamu kila mahali..kuanzia ukataji misitu kwenye maeneo ya kitropiki hadi uvuvi kupitia kiasi kwenye bahari…kuanzia ongezeko la uhaba wa maji safi hadi uchafuzi wa anga na bahari, ardhi na maji maeneo mengi duniani….kutokomea kwa bayonuai hadi ongezeko la mabadiliko ya tabianchi.”

Ban ametaka kila sekta na kila nchi kushirikiana kudhibiti mabadiliko ya tabianchi na kuendeleza maendeleo endelevu. Mkutano wa UNEA unatarajiwa kuibuka na azimio la utekelezaji.

Kesho Jumamosi Ban atashiriki tukio maalum la kuangazia umuhimu wa ubia wa sekta ya umma na ile binafsi katika kupatia suluhu matatizo yanayokabili binadamu.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter