Kukosa makazi, hofu na ufukara sasa vimetawala kwenye maisha ya watoto wa Iraq waliokimbia makazi yao kufuatia mapigano ya wiki mbili zilizopita nchini humo, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF.
Mwakilishi wa shirika hilo huko Iraq, Marzio Babille akizungumza baada ya kutembelea mji wa Tel Keif ulioko kilometa kadhaa kaskazini mwa mji wa Mosul uliotwaliwa na waislamu wenye msimamo mkali, amesema nyuso za watoto zinadhihirisha hofu waliyo nayo.
UNICEF inasema watu walioshuhudia machungu kutokana na vita vya Iraq walidhania kuwa hawatopata tena majinamizi hayo lakini sasa taarifa za mapigano zinawafanya wakimbie huku na kule.
Pamoja na kuhofia athari za kisaikolojia kwa watoto kutokana na mapigano hayo, Babille anasema wanahofia pia uwezekano wa kuibuka kwa magonjwa msimu huu wa kiangazi unapoanza.
Tangu kuanza kwa mapigano ya hivi karibuni, UNICEF imeshasambaza lita Laki Moja za maji safi na salama ya kunywa, vifurushi 5,000 vya vyakula na vingine 3,500 vya vifaa vya kujisafi.
UNICEF inasema hofu yake pia ni kwamba mapigano yanaendelea na hivyo watashindwa kufikisha mahitaji ya kibinadamu kwa watoto walioko kwenye maeneo ambayo bado hayajafikiwa kutokana na kuzorota kwa usalama.
Hofu nyingine ni ripoti ya kwamba watoto wanaingizwa kwenye mapigano bila kujali usalama na ustawi wao na kwamba kitendo hicho ni kinyume na sheria za kibinadamu za kimataifa.
UNICEF imerejelea wito wake kwa pande zote kwenye mzozo wa Iraq kuzingatia wajibu wao wa kulinda watoto.