Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Raia zaidi wa Ukraine wafurushwa wakati mzozo ukitokota

Mwanamke akikunja nguo katika kliniki moja huko Ukraine inayowapokea wakimbizi wa ndani kutoka Crimea. Picha: UNHCR//N.Dovga

Raia zaidi wa Ukraine wafurushwa wakati mzozo ukitokota

Watu 16,000 zaidi nchini Ukraine wamelazimika kuhama makwao na kukimbilia maeneo mengine ya nchi katika kipindi cha wiki moja iliyopita, limesema Shirika la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR, ambalo linakadiria kuwa takriban watu 54,000 wamelazimika kuhama ndani ya nchi hiyo.

Watu 12,000 katika idadi hiyo nzima ni kutoka katika eneo la Crimea, na wengine wanatoka eneo la mashariki la nchi. UNHCR pia inasema kuwa watu zaidi wanakimbia Ukraine na kuvuka mpaka kuingia Urusi na nchi nyingine, ingawa sasa ni idadi ndogo tu ya watu hao ndio wameomba kuchukuliwa kama wakimbizi.

Melissa Fleming ni msemaji wa UNHCR:

“Kuongezeka kwa idadi ambayo tumeona wiki iliyopita inasadifiana na kuzorota kwa hali hivi karibuni mashariki mwa Ukraine. Watu waliolazimika kuhama wanataja kudhoofika kwa sheria na utaratibu, na wanasema kuwa wanaogopa kutekwa nyara na kwamba kuna ukiukwaji wa haki za binadamu, pamoja na kuvurugika kwa huduma za umma. Wengine pia wanaripoti kuwa wamepoteza risiki zao.”

Tangu mwanzoni mwa mwaka huu, takriban raia 110,000 wa Ukraine wamewasili Urusi, na 750 wameomba hifadhi salama katika nchi za Poland, Belarus, Jamhuri ya Czech na Romania. Ni 9,600 tu walioko Urusi ndio wameomba hifadhi salama. Watu wengi wanajaribu kusaka njia ya kuishi nchini kinyume na sheria, wakihofia kutatizika iwapo watataka kurejea Ukraine.