Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ulinzi wa kijamii waboresha maisha ya watu wanaoishi na HIV: ILO

Ulinzi wa kijamii waboresha maisha ya watu wanaoishi na HIV: ILO

Shirika la kazi duniani, ILO limezindua  ripoti yake inayoonyesha kuwa watu wanaoishi na virusi vya ukimwi wana uwezo wa kuishi maisha bora zaidi iwapo wana ulinzi wa kijamii. John Ronoh na taarifa kamili.

(Taarifa ya John)

Ripoti hiyo ikizingatia utafiti uliofanywa Guatemala, Indonesia, Rwanda na Ukraineambazo ziko kwenye orodha ya Umoja wa Mataifa ya nchi zilizoathirika zaidi na Ukimwi au zinaimarisha mifumo yake ya hifadhi ya jamii.

Ilibainika kuwa kwenye nchi hizo asilimia kati ya 63 na 95 ya watu wanaoishi na virusi vya ukimwi na ambao wako kwenye mfumo wa hifadhi ya jamii wana uwezo wa kuendelea na ajira zao au kushiriki kwenye shughuli za uzalishaji.

Halikadhalika watu hao pia waliripoti kuwa watoto wao waliweza kuendelea na shule huku kiasi kikubwa pia kikiwa na uwezo wa kupata dawa za kupunguza makali ya virusi vya Ukimwi.

Jean-Luc Martinage ni msemaji  wa ILO mjini Geneva, Uswisi.

 “Ujumbe wa msingi wa ILO ni kuendelea kuwekeza pesa katika mifumo ya hifadhi na ulinzi wa kijamii ambayo itajumuisha watu wote, hasa watu walioathirika na virusi vya ukimwi na wanaoishi kwenye mazingira hatarishi.”

 ILO inasema upatikanaji wa dawa hizo unawezesha watu kuishi, lakini kama hakuna mpango maalum ya ulinzi kwa  wanaume, wanawake na jamii zao, hali hii  itawafanya dhaifu  na maskini .