Kudhibiti Ebola yahitaji mshikamano wa nchi zote Afrika Magharibi: WHO

26 Juni 2014

Shirika la Afya Duniani, WHO limehimiza harakati za pamoja zichukuliwe ili kudhibiti kuenea kwa kirusi cha Ebola katika Afrika Magharibi ambapo ugonjwa huo umeendelea kusambaa nchini Guinea, Liberia na Siera Leone.

Shirika hilo limetoa msaada kwa kutuma kundi la Wataalamu 150 wenye ujuzi tofauti ili washiriki shughuli mbali mbali za kupambana na mkurupuko wa ugonjwa huo, kama utafiti na uchunguzi, mawasiliano, kudhibiti maambukizi, utaratibu wa ugavi na usafirishaji, pamoja na kukusanya takwimu na maelezo.

Licha ya hayo, kumekuwa na ongezeko kubwa la maambukizi mapya na vifo kutokana na Ebola, na ripoti zinaonyesha kwamba wilaya zingine mpya zimekumbwa na shida hiyo kwa wiki tatu zilizopita.

Kufikia tarehe 23 Juni, visa 635 viliripotiwa ambapo 399 kati yao wamefariki dunia.  Hii imefanya mkurupuko huo kuwa ndio mkubwa zaidi, kutokana na idadi ya vifo maambukizi na vifo, na pia eneo la kusambaa maambukizi.

Daktari Luis Sambo, Mratibu Msimamizi wa Shirika la Afya, ukanda wa bara la Afrika amesema kuwa janga hili sasa sio tu la nchi mmjoa, bali ni jambo linalohitaji kuangaziwa na serikali zote katika eneo hilo na wadau. WHO imeelezea hofu yake kuwa watu kuendelea kuvuka mpaka huenda kukasambaza ugonjwa huo katika nchi jirani na hata kuyaeneza maambukizi katika viwango vya kimataifa.

Ili kudhibiti usambazaji wa virusi vya Ebola, Shirika la Afya duniani limeitisha mkutano wa dharura mnamo tarehe 2 hadi 3 Julai mjini Accra, Ghana ukijumuisha mawaziri wa afya wa nchi 11 na wadau wengine, ili kujadili mbinu za kukabiliana na tatizo hilo, na pia kuweka mikakati ya kina na shirikishi yenye lengo la kudhibiti hali iliyoko sasa na hata siku za usoni.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter