Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama laombwa kusaidia maisha ya watu milioni 10.8 Syria

Valerie Amos

Baraza la Usalama laombwa kusaidia maisha ya watu milioni 10.8 Syria

Mkuu wa Ofisi ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu katika Umoja wa Mataifa, Valerie Amos, amelihutubia Baraza la Usalama leo, akimulika ripoti ya nne kuhusu hali ya kibinadamu nchini Syria tangu kupitishwa kwa azimio namba 2139 la kuruhusu kufikishwa kwa misaada ya kibinadamu kwa walengwa nchini humo.

Bi Amos amesema mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau wa kibinadamu wameendelea kufanya juhudi zao za kukidhi mahitaji ya dharura ya kibinadamu, huku wahudumu wakipelekwa kwa maeneo magumu na hatarishi ili kufanya mazungumzo ya kutafuta uwezekano wa kufikisha misaada inayohitajika.

“Wengi wao wameuawa, kujeruhiwa, kuzuiliwa au kutekwa nyara. Takriban wahudumu 60 wa kibinadamu wamepoteza maisha wakiwa wanatimiza majukumu yao kufikia sasa. Muda mwingi umepotezwa kutafuta njia ya kuwezesha misafara ya misaada, katika mazingira ya utaratibu mgumu wa kiutawala. Licha ya juhudi hizi zote, tukiwa katika mwaka wa nne wa vita hivi sasa, hatuwezi kuwafikia kwa njia endelevu takriban nusu ya watu waliotambuliwa kuwa wenye mahitaji ya dharura zaidi”

Bi Amos amesema, ukosefu wa usalama na mapigano kuendelea, kunachangia kuzuia kufika kwa misaada ya kibinadamu katika maeneo mengi, huku akiongeza kuwa mahitaji yanazidi kuongeza na kuzidi uwezo wa kuyaitikia.

“Bado hatuwezi kutoa msaada wa mara kwa mara na kwa njia endelevu kwa watu milioni 4.7 katika maeneo magumu kufikia. Baraza hili limeyataka makundi yanayozozana yaruhusu na kuwezesha kufikisha huduma za kibinadamu, kupita ngome za vita na mipakani. Azimio 2139 ni dhahiri kuhusu hili. Tunahitaji kuongeza usafirishaji wa misaada ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka.”

Bi Amos amesisitiza udharura wa hali wanaokabiliana nao, na kulitaka Baraza la Usalama kusaidia katika kuhakikisha kuwa pande zinazozozana zinatimiza wajibu wao chini ya sheria ya kimataifa, kwani watu milioni 10.8 wanategemea msaada huo wa Baraza la Usalama.