Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Harakati za kuwaandikisha watoto shuleni zakumbwa na mkwamo

@UNICEF Tanzania/Holt 2014

Harakati za kuwaandikisha watoto shuleni zakumbwa na mkwamo

Ripoti mpya ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi, na Utamaduni, UNESCO, inaonyesha kwamba kasi ya uandikishaji wa watoto shuleni imekwama tangu 2007, idadi ya watoto wasiokuwa shuleni ikiwa ni milioni 58, na nusu yao wakiwa Afrika.

Mkuu wa UNESCO, Irina Bokova, ameeleza kwamba, ufadhili katika sekta ya Elimu umeendelea kupungua, na hofu kubwa ni kwamba nchi nyingi hazitatimiza lengo la maendeleo la milenia la Elimu kwa Wote ifikapo mwaka 2015.

Amesema, utashi wa kisiasa unatakiwa ili kurejesha watoto hawa shuleni. Changamoto kubwa ni gharama za elimu zinazochangishwa kwa wazazi, takwimu zikionyesha kwamba, serikali ikiwekeza dola mia katika sekta ya elimu, hua mzazi anatakiwa kuchangia pesa kwa ajili ya ada za masomo, sare, vitabu, na kadhalika, kuanzia dola kumi ikiwa ni Marekani hadi dola 70 nchini Benin.

Katika ripoti yake, UNESCO imetolea mifano ya nchi 17, ambazo zimefanikiwa kupunguza sana idadi ya watoto walio nje ya shule, kwa kutumia harakati mbali mbali, kama mfano kuongeza bajeti ya elimu, kuboresha mtalaa, kufundisha kwa lugha za mama ama kuondoa ada za shule.