Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afghanistan: UM wahofia uchaguzi wachafua hali ya utulivu

Afghanistan: UM wahofia uchaguzi wachafua hali ya utulivu

Jan Kubis, mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan na Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, UNAMA, alihutubia baraza la Usalama leo kupitia mfumo wa video na kuripoti kuhusu matokeo ya duru ya pili ya uchaguzi wa urais iliyofanika tarehe 14, Juni.

Mamilioni ya raia wa Afghanistan walijitokeza katika uchaguzi uliokuwa wa kwanza katika mfumo wa kidemokrasia baada ya mwisho wa mzozo, lakini visa vya uhalifu na ugaidi vimeripotiwa siku hiyo, vikisababisha mgombea mmoja kujitoa kwa utaratibu huo akikiri kuwepo kwa udanganyifu na uwongo kwa wingi.

Jan Kubis ameziomba pande zote za uchaguzi kuwajibika na kuachana na maneno ya kikabila, akisema, anayeshinda uchaguzi ni mtu mmoja tu. Hatimaye, aliwatakia raia wa Afghanistan Ramadhan Kareem, akiwaomba kuchukua nafasi ya mwezi wa Ramadhani kurejesha hali ya usalama na upendo nchini humo.

Halikadhalika, Yuri Fedotov, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na udhibiti wa dawa za kulevya na uhalifu UNODC, amelielezea Baraza la Usalama kwamba nchi ya Afghanistan inategemea biashara ya madawa ya kulevya, biashara hiyo ikichangia kwa asilimia 10 hadi 15 ya ukuaji wa uchumi, licha ya jitihada zilizofanyika na mamlaka za serikali. Amesema, asilimia 80 ya madawa ya heroini na afiuni duniani inatoka Afganistan.

Hatimaye, baraza la usalama limewaomba wagombea wa urais kuonyesha subira na heshima katika utaratibu wa uchaguzi ili kutunza hali ya utulivu, na pia limeiomba jamii ya kimataifa kuongeza ushirikiano ili kupambana na biashara haramu ya madawa ya kulevya.