Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkurugenzi wa WFP atathmini mahitaji ya kibinadamu Kaskazini mwa Iraq

Picha: WFP

Mkurugenzi wa WFP atathmini mahitaji ya kibinadamu Kaskazini mwa Iraq

Mkurugenzi mkuu was shirika la mpango wa chakula duniani WFP Ertharin Cousin amehitimisha ziara yake ya siku mbili nchini Iraq ambako pamoja na mambo mengine  amekutana na familia zilizokimbia mapigano katika mji wa Mosul .Taarifa kamili na George Njogopa

TAARIFA YA GEORGE

Katika ziara yake hiyo Cousin alitembelea kambi ya muda ya Kalak na kukutana na mamia ya raia waliokimbia mapigano huko Mosul.Akizungumza mwishoni mwa ziara yake Cousin ametaja hali ngumu wanayokumbana nayo wakazi wa eneo hilo, akisema kuwa ni wale tu wenye nguvu na bahati ndio wanaoweza kutembea mwendo mrefu au wenye uwezo wa kusafiri kwa gari ndio wanaoweza kwenda kwenye kambi ya  Kalak.

Amesema pamoja na kukumbwa na madhila ya vita, familia nyingi zinakabiliwa na ukosefu wa huduma muhimu ikiwamo chakula.

Ameeleza kuwa raia hao wameyarejelea upya maisha ya shida na dhiki na kwamba baadhi yao wamelazimika kukimbilia maeneo yasiyojulikana jambo ambalo ni hatari kubwa Kwa usalama wao. WFP imezindua operesheni ya dharura kuwapa chakula zaidi ya watu nusu milioni ambao wameathiriwa na mapigano ya sasa Iraq, huku ikikabiliwa na changamoto za usalama na ufadhili.