Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkurupuko wa Ebola Afrika ya Magharibi waendelea

Mkurupuko wa Ebola Afrika ya Magharibi waendelea

Homa ya ebola inaendelea kuambukiza mamia ya watu katika ukanda wa Afrika ya magharibi ambapo Shirika la Afya Duniani WHO linahofia kutoweza kudhibiti ugonjwa huo. Taarifa zaidi na Amina Hassan.

(Taarifa yaAmina)

Akizungumza na waandishi wa habari leo mjini Genva, Fadela Chaib, msemaji wa WHO amesema mkurupuko huo wa Ebola unazidi kusambaa Guinea, Liberia na Sierra Leone.

" Hali inatia wasiwasi, ni mara ya kwanza kwa historia ya Ebola kuona ugonjwa unaoambukizwa kutandaa katika nchi tatu kwenye ukanda ambao haujawahi kushuhudia visa vya Ebola. Pia jamii imekuwa na tabia ya kutofuatilia sheria za kuzuia maambukizo. Ebola haijadhibitiwa, visa vinaripotiwa kila siku, na vifo pia kwa bahati mbaya.”

Tayari WHO kwa kushirikiana na madaktari wasio na mipaka wameongeza jitihada za kupambana na maambukizo na kujaribu kuokoa maisha ya waathirika, kwa kutuma watalaam wengi zaidi huko.

Karibu visa 600 vimeripotiwa kwenye nchi hizo tatu na watu 369 wamefariki dunia . WHO imesisitiza ni muhimu watu wajitahadhari na maambukizo, hususan kwenye misiba.