Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mfuko wa ujenzi wa amani umepata ufanisi mkubwa: Eliasson

Jan Eliasson, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. (Picha@ UN /Paulo Filgueiras)

Mfuko wa ujenzi wa amani umepata ufanisi mkubwa: Eliasson

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Jan Eliasson, ametoa wito kwa nchi wanachama zitimize ahadi zao za kuufadhili mfuko wa ujenzi wa amani, akisema kuwa mfuko huo umetimiza mengi tangu ulipozinduliwa. Joshua Mmali na taarifa kamili

(Taarifa ya Joshua)

Akiuhutubia mkutano wa nne wa ngazi ya juu wa wadau wa mfuko wa ujenzi wa amani, Bwana Eliasson amesema mfuko huo ulizinduliwa kwa minajili ya kuboresha jinsi Umoja wa Mataifa unavyozisaidia nchi zinazoibuka kutoka katika migogoro.

Amesema lengo lilikuwa na kuwezesha Umoja wa Mataifa kuchukua hatua haraka, kuingilia kati kwa njia inayofaa zaidi na kuzisaidia nchi hizo kupiga hatua nzuri zaidi za kuondokana na migogoro na kuelekea amani.

Ameongeza kuwa mfuko huo umesaidia kujenga ushirikiano baina ya Umoja wa Mataifa na mashirika ya kimataifa ya fedhakamavile Benki ya Dunia, na kuboresha ushirikiano ndani ya mfumo wa Umoja wa Mataifa. Pia mfuko huo umewezesha wadau wa kitaifa kujenga taasisi thabiti za kifatia ambazo ni msingi wa amani unahitajika.

Amesema tangu ulipozinduliwa, mfuko huo umepata ufadhili wa zaidi ya dola nusu bilioni, na kuweza kutumia zaidi ya dola milioni 490. Hata hivyo, amesema ufadhili zaidi utahitajika

“Natoa wito kwa wafadhili wa mfuko huu kutimiza ahadi zao, hususan kutokana na matokeo mazuri ya tathmini ya matumizi yake kote duniani.Mfuko wa ujenzi wa amani upo kuthibitisha kuwa hapawezi kuwa na amani bila maendeleo, na hapawezi kuwepo maendeleo bila amani, na kwamba mawili hayo hayawezi kuendelezwa bila kuheshimu haki za binadamu.”