Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sabuni za kusugua mwili zahatarisha viumbe vya baharini na binadamu: UNEP

@ Peter Prokosch, GRID Arendal

Sabuni za kusugua mwili zahatarisha viumbe vya baharini na binadamu: UNEP

Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa, UNEP, limeelezea wasiwasi wake kuhusu hatari mpya itokanayo na takataka za plastiki ndogondogo ambazo zinahatarisha maisha ya viumbe vya baharini.

Katika ripoti yake kuhusu hasara za takataka za plastiki na umuhimu wa kuzihuisha, UNEP imesema plastiki hizo zinapatikana zaidi siku hizi kwenye madawa ya meno ama sabuni za kusugua mwili, ikisema hazichujiki kwa kutumia vifaa vya uhuishaji wa kawaida.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa viumbe vingi vya baharini humeza takataka hizo na hivyo husambaa kwenye mtandao wa chakula hadi kwa binadamu na husababisha magonjwa mbalimbali.

UNEP inasema suluhu la haraka ni kuhuisha plastiki kwani inawezekana na hatua zinazohitajika kuchukuliwa ni pamoja na kampuni kutakiwa kutoa taarifa kuhusu utumiaji wa plastiki, zipunguze matumizi ya plastiki na vile vile kuendelea kuelimisha jamii kuhusu microplastiki na jinsi ya kuzuia plastiki kuingia baharani.