Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kifo cha mume kisiwe kibali cha kushusha hadhi na utu wa mwanamke: Ban

Katibu Mkuu wa UM Ban Ki-Moon. Picha @UN-Maktaba

Kifo cha mume kisiwe kibali cha kushusha hadhi na utu wa mwanamke: Ban

Hakuna mwanamke anapaswa kupoteza hadhi, utu, ustawi au kipato chake eti kwa sababu amefiwa na mumewe, ni kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon katika siku ya wajane duniani hii leo.

Ban amesema suala hilo ni dhahiri lakini bado mamilioni ya wanawake duniani wanakumbwa na manyanyaso, ukatili na hata kuenguliwa kwenye urithi wa mali pindi wanapofiwa na waume zao.

Ametolea mfano suala la wanawake kuchomwa moto au kurithiwa na ndugu za waume zao kwa fikra potofu ya kuwatakasa akisema kuwa mila hiyo inachukiza, imepitwa na wakati na inaongeza uwezekano wa mjane kuambukizwa virusi vya HIV.

Ban amesema athari hizo zinagusa pia watoto wa mjane pamoja na ndugu wanaotemtegemea.

Katibu amesema ni jukumu la kila mtu kulinga haki za binadamu na utu wa wajane kwa mujibu wa mkataba wa kimataifa wa kutokomeza ubaguzi dhidi ya wanawake na ule wa haki za mtoto.

Amesema katika siku hii ya leo ni vyema kila mtu kuahidi kuchukua hatua thabiti kuwezesha wanawake, kuendeleza usawa wa kijinsia na kutokomeza aina zote za ukatili dhidi ya wanawake.

Ban amesema kwa pamoja dunia inaweza kutokomeza changamoto zinazokumba wajane duniani kote na kuwawezesha kufikia fursa zao kama washirika sawa kwenye jamii.