Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto ni wahanga wa wimbi jipya la machafuko Iraq: Zerrougui

Leila Zerrougui

Watoto ni wahanga wa wimbi jipya la machafuko Iraq: Zerrougui

 Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu kuhusu Watoto na Mizozo ya Silaha, Leila Zerrougui, ameelezea kusikitishwa na kuongezeka kwa machafuko hivi karibuni katika mzozo wa Iraq, na kutoa wito kwa makundi husika kuwalinda watoto na kuchukua hatua zote zinazohitajika kukomesha mara moja na kuzuia ukatili wote unaotendwa dhidi ya watoto.

Bi Zerrougui amesema katika taarifa kuwa amepokea habari za kutia wasiwasi kwamba watoto wanahusishwa katika mzozo huo, na kueleza kusikitishwa na athari za machafuko hayo dhidi ya watoto.

Mnamo mwaka 2013, watoto 3 waliuawa kila siku katika mashambulizi, kwa mabomu na kufyatuliana risasi, idadi hiyo ikiwa imezidi ile ya watoto waliouawa au na kulemazwa mnamo mwaka 2012.

Bi Zerrougui amesema kuwa wimbi la machafuko ya hivi karibuni huenda likawadhuru watoto wengi hata zaidi, wakiuawa, kujeruhiwa, kulazimika kuhama makwao au kutenganishwa na familia zao. Amesema idadi ya watoto wanaouawa katika mashambulizi dhidi ya raia ambayo yanatekelezwa na kundi la ISIS na makundi mengine yaliyojihami na pia vikosi vya serikali, inaongezeka kwa viwango vya kutia hofu.