Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Awamu mpya ya chanjo dhidi ya polio yaanza Syria

Picha: UNICEF/Ayberk Yurtsever (UN News Centre)

Awamu mpya ya chanjo dhidi ya polio yaanza Syria

Shirika la Afya Duniani, WHO, na Shirika la Kuhudumia Watoto, UNICEF, yamesema yatasaidia awamu nyingine ya zoezi la utoaji chanjo dhidi ya polio nchini Syria, ambalo linaanza wiki hii, kama sehemu ya juhudi za kikanda za kukabiliana na kuenea kwa kirusi kinachosababisha ugonjwa wa kupooza viungo vya mwili Mashariki ya Kati.

Kampeni hiyo, ambayo ni ya nane nchini Syria, inalenga kuwafikia watoto milioni 2.8 kote nchini katika siku 5 zijazo, wakiwemo wale walioko kwenye maeneo yanayozozaniwa na magumu kufikiwa.

Meneja wa Kutokomeza polio katika WHO, Chris Maher, amesema wanaongeza juhudi za kuhakikisha kuwa kila mtoto chini ya umri wa miaka mitano anapokea dozi kadhaa za chanjo ya polio. Mwezi uliopita, WHO ilitangaza polio kuwa tatizo la kiafya la dharura lenye tishio la kimataifa. Ugonjwa huo unaweza kuzuilika kwa urahisi, ingawa unaweza kuenea kwa kasi ikiwa watoto hawakupata chanjo na kinga dhidi yake.