Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Eritrea yatoswa kidole cha lawama kuhusu hali ya haki za binadamu

UN Photo/Amanda Voisard
Sheila Keetharuth.

Eritrea yatoswa kidole cha lawama kuhusu hali ya haki za binadamu

Mtaalam maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Eritrea, Sheila B. Keetharuth, ametoa wito kwa Baraza la Haki za Binadamu na jamii ya kimataifa kukabiliana na ukiukwaji wa haki za binadamu wa mara kwa mara nchini Eritrea, ambao unawalazimu takriban watu 2,000 kuikimbia nchi hiyo kila mwezi kwenda Ethiopia, na takriban watu 2,000 waliokimbilia Sudan mwezi Mei mwaka huu wa 2014.

Bi Keetharuth amesema hayo wakati akiwasilisha ripoti yake kuhusu hali ya haki za binadamu nchini humo kwa Baraza la Haki za Binadamu, ambalo linafanya mikutano ya kikao chake cha 26 mjini Geneva, Uswisi.

Mtaalam huyo wa haki za binadamu amesema kukimbia kwa halaiki ya watu hao, wakubwa kwa wadogo, kunaweza kupungua ikiwa kutowajibishwa kisheria kwa ukiukwaji wa haki za binadamu kutakomeshwa. Amesema kuna haja ya kuboresha uwanja wa haki za binadamu nchini Eritrea, kwani hali ni mbaya mno, na hakuna muda wa kupoteza.

Baadhi ya vitendo vilivyotajwa katika ripoti hiyo ni pamoja na kuwashurutisha raia kutoa huduma kwa taifa kwa kipindi kisichokuwa na kikomo, na tatizo linaloendelea la ukamataji watu kiholela na kuwazuilia katika mazingira hatarishi.

Mwakilishi wa Eritrea kwenye Baraza hilo amekanusha yaliyomo kwenye ripoti hiyo, akisema ni madai ya kisiasa ambayo yanajisitiri katika haki za binadamu, akiongeza kuwa taifa lake limekuwa mhanga wa ajenda ya kisiasa kimataifa.